Mwanzoni mwa Oktoba hii, Rais Jakaya Kikwete alitoa kauli iliyopokelewa vyema na uongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) kuhusiana na utatuzi wa mgogoro wa kisiasa Zanzibar lakini ikapokewa vibaya na uongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) inayoongozwa na Chama chake cha Mapinduzi (CCM).

Rais Kikwete alikuwa amesema, kwa ufupi na kwa mkato, kwamba suala la kuushughulikia mpasuko wa kisiasa wa Zanzibar limefika pazuri. Mbio mbio, uongozi wa CUF ‘ukaichangamkia’ kauli hiyo kwa kusema kwamba inatia moyo na unaamini Rais Kikwete atatimiza ahadi na jukumu lake. Bali hata ukaenda mbali zaidi kukiri kujuwa uwepo wa mazungumzo yasiyo rasmi baina ya pande husika huku ukimtaja Rais Amani Karume kuwa ‘anaanza kubadilika’.

Lakini siku ya tatu yake, ikaripotiwa kwamba SMZ inasema kinyume kabisa ya kile kilichosemwa na Rais Kikwete (au angalau kile kilichotafsiriwa kutokana na kauli ile ya Rais Kikwete). Kwamba hakuna kabisa suala kama la kuwa na “serikali ya mseto” Zanzibar. Kwamba “uchaguzi ulishafanyika” na “mwengine utakuja 2010” na kwamba “lililobaki ni kujenga nchi” tu. Naibu Waziri Kiongozi na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo wa SMZ, Ali Juma Shamuhuna, ndiye aliyeyasema hayo.

Hapa pana mitazamo mitatu kuhusiana na kauli hizi mbili zinazopingana za uongozi wa serikali na CCM, baina ya Bara na Zanzibar, ambayo makala hii inadhamiria kuichambua. Masuala ya msingi ya kujiuliza ni ikiwa (kwa kutumia mtazamo wowote ule kati ya hiyo mitatu) msimamo wake unamaanisha nini kwa mwenendo wa siasa na maendeleo ya nchi, nani aliyeujenga na anayefaidika nao na nini hatima yake.

Mtazamo mmoja ni kwamba kile alichokisema Shamuhuna ndio msimamo wa SMZ na kwamba aliwakilisha hoja ya wahafidhina wa Zanzibar kama inavyotakiwa. Kwa mtazamo huu, Shamuhuna hakusema kama Shamuhuna, bali kama CCM Zanzibar na kama SMZ.

Ikiwa mtazamo huu uko sawa, na uwezekano huo upo, hakuna jipya katika hilo. Utakuwa ni muendelezo tu wa kile kilichozoeleka. Kwamba huo ndio umekuwa msimamo wa wahafidhina hawa kwa miaka yote hii na hakuna chochote ambacho ungelitegemea kitoke vinywani mwao pungufu ya kauli kama hii. Mahodari wa kutishia nyamarero kila pale wanapohisi kuwa kuna maamuzi ambayo yatawatwaza.

Utetezi wa Rais Karume kwa kauli hiyo ya Shamuhuna dhidi ya hoja ya Mohammed Seif Khatib (waziri wa Serikali ya Muungano-SMT mwenye dhima sawa na Shamuhuna) katika kikao kilichofanyika kwenye wiki ya mwanzo ya mwezi huu Kisiwandui, Zanzibar, kwamba “Rais Kikwete hakueleweka……. anachokizungumzia sio serikali ya mseto”, (angalia Tanzania Daima la Oktoba 9, 2006) ni mfano kwamba hivyo ndivyo wanavyosema wahafidhina wetu.

Lakini ikiwa msimamo huo wa wahafidhina wa SMZ sio msimamo wa SMT (na katika muktadha huu pia wa CCM Bara), basi hakuna la kuhofia. Na sababu ya kutohofia ni nyepesi sana – ni ukweli kuwa uongozi hasa wa Tanzania, ikiwemo Zanzibar, uko Chimwaga!

Historia ya kisiasa ya nchi hii imejaa mifano inayoshuhudia kwamba maamuzi yote magumu na muhimu ya kuiendesha Zanzibar hayajawahi kufanyika na kufanikishwa na vikao vya Kisiwandui wala vya Mnazi Mmoja.

Mifano hiyo inajumuisha Mapinduzi ya 1964, matukio na matokeo ya kuchafuka kwa hali ya kisiasa Zanzibar mwanzoni mwa miaka ya ’80 na hata kupatikana kwa mgombea uraisi na raisi wa Zanzibar katika miaka iliyofuatia hapo. Wimbo kwamba: “CCM ina wenyewe” unasema ukweli mtupu kabisa. Na hapa wacha tuangaliane machoni tupate kuambiana ukweli, kwamba wenyewe hao si akina Shamuhuna.

Akina Shamuhuna hawa hawa walisimama kidete kutaka katiba ibadilishwe ili Rais wa Awamu ya Tano, Dk. Salmin Amour, aendelee kugombea nafasi hiyo hata baada ya kipindi chake cha miaka kumi kumalizika na waliposhindwa hilo, wakapigania mteule wa Salmin, Dk. Mohammed Gharib Bilal, awe mgombea wa nafasi hiyo. Yote yalizimwa na Chimwaga.

Lakini mtazamo wa pili ndio hasa wa kutia hofu. Huu ni uwezekano kwamba, alichokisema Shamuhuna ni mkakati wa pamoja baina ya CCM Zanzibar na CCM Bara, na hivyo kauli yake inawakilisha pia msimamo wa Chimwaga. Yaani, kimkakati, hivyo ndivyo CCM kwa ujumla wake ilivyokubaliana – huku Rais Kikwete atowe kauli za matumaini ambazo zitaweza kuununua na kuupitisha muda na kule akina Shamuhuna waeleze ukweli hasa kama ulivyo ili kujenga morali na mshikamano wa chama.

Na hili nalo ni rahisi kuliona kwa kuzingatia mifano mingi tu, kuanzia kupotea kwa watu katika mazingira ya kutatanisha katika awamu za mwanzo za utawala hadi kuvunjika kwa Muwafaka wa 2001. Katika awamu ya mwanzo ya utawala Zanzibar, ambapo pia ilikuwa ni mwanzoni mwa awamu ya mwanzo ya utawala Bara, watu wengi walipotea Zanzibar katika mazingira ya kutatanisha mbele ya macho ya SMT. Bali kuna mifano mibaya zaidi, kama ule wa Abdallah Kassim Hanga, ambapo SMT iliwapeleka watu Zanzibar ikijuwa fika kwamba nao wanakwenda ‘kupotea’.

Muafaka wa 2001 uliambiwa kwamba ungelikufa kabla ya 2005 na waliosema hivyo ni watu wa kawaida kutoka CCM Zanzibar, kama vile Hafidh Ali Tahir, siku hizo akiwa mwakilishi wa Jimbo la Rahaleo, Zanzibar. Na hivyo ndivyo ilivyokuwa. Sitaki kuamini kuwa uongozi wa SMT wa wakati ule haukuisikia kauli ile. Na ndio pia sitaki kuamini ikiwa SMT haikushiriki kuua Muwafaka wa 2001 katika kiwango kile kile ilichoshiriki kuumba, hata kama uongozi huo ulikuwa ukipita na kujinadi kwa mabalozi kwamba umejitolea kuutekeleza Muwafaka wote kipengele kwa kipengele. Yaliyofanyika katika uchaguzi wa 2005 ndiyo yanayonifanya nisiamini hivyo. Na kwa mujibu wa mtazamo huu, basi si ajabu sana ikiwa na hili la Shamuhuna linawezekana.

Halafu kijembe kilioje ni kwamba, inapotokea hali kama hizo, uongozi wa SMT hukaa chonjo na kujifanya hauhusiki kabisa na yale yanayotokea Zanzibar. Mfano ni maelezo ya Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa, kwa Jonathan Powers kwenye jarida la The Prospect la Agosti 2004 kwamba, wenzake wa Zanzibar walikuwa tayari hata kuua lakini waendelee kubakia madarakani. Mfano pia ni kauli ya Waziri Mkuu, Edward Lowassa, katika kikao cha Bunge kilichopita kwamba licha ya SMT kuujuwa uvunjwaji wa haki za binaadamu unaofanywa na vikosi vya SMZ Zanzibar, lakini haiwezi kulishughulikia suala hilo hadi hapo Tume ya Haki za Binaadamu itakapoanza kufanya kazi zake huko.

Haya ni majibu yanayokinzana na wakati huo huo kuonesha uhalisia ulivyo. Katika upande mmoja, uongozi wa SMT unajitenga uovu unaotendeka Zanzibar, lakini kwa upande mwengine unajishirikisha nao kwa kuonesha utowajibikaji.

Kwa Mkapa kusema tu kwamba wenzake wa Zanzibar walikuwa tayari hata kuua, lakini asichukuwe hatua yoyote kuwazuia wasiue na kwa Lowassa kusema kwamba Wazanzibari hawawezi kulindiwa usalama wa maisha yao na mali zao kwa kuwa Tume ya Haki za Binaadamu haijaruhusiwa kuwapo Zanzibar, hayakuwa maelezo ya bahati mbaya. Ni mifano tu inayoonesha namna gani serikali hizi mbili (SMZ na SMT) hushirikiana kwa ‘staili’ zao kuibakisha Zanzibar mahala ilipo.

Kwa mtiririko huo huo, Rais Kikwete anaweza kuja mwishoni mwa utawala wake na kusema kwamba: “unajuwa kulre Zanzibar kuna utawalra wake wenyewe. Nisingeweza kufanya chochote ambacho watawalra wa kulre hawakitaki..”. lakini wakati huo huo akija akiona kuna hatari ya watawala hao kuondolewa kwa nguvu ya umma, akapeleka majeshi kama alivyoyapeleka mwenzake Mkapa kuwalinda.

Mtazamo wa tatu na wa mwisho ni kwamba, kauli ya Shamuhuna haikuwa ikiwakilisha msimamo hata mmoja kati ya hiyo miwili, yaani si ya SMT na CCM Zanzibar wala ya SMT na CCM Bara na hivyo amejisemea tu ‘kivyakevyake’. Uwezekano wa hili nao pia upo maana una sababu zake.

Shamuhuna ni katika wanasiasa wanaoweza kuwekwa katika lile kundi la controversial. Hilo haliondoi ukweli kwamba, ni mwanasiasa mwenye satwa, lakini ameipata satwa hiyo kwa kutumia mbinu na hila nyingi. Anajuilikana kwa ‘ukaskazini’ wake na kwamba hiyo ni katika nyenzo za uwanasiasa wake. Anajuilikana pia kwa uchapakazi wake usio mfano na uwezo wake wa kulisema alitakalo. Na mwisho anajuilikana pia kwa uwezo wake wa kugeuka.

Kwa mfano, licha ya kuwa mpinzani mkubwa wa utawala wa Rais Karume katika kipindi kilichopita, aliweza baadaye kujinyumbua kama amoeba na kujiweka katika mazingira ya kukubalika ndani ya ‘waliomo’ kwenye utawala huo mara tu kipindi chengine kilipoanza. Sasa, husemi ila si yeye aliyekuwa akipinga kila jambo na mambo yote wakati ule alipokuwa mwakilishi tu katika Baraza la Wawakilishi. Hivi sasa ni mtetezi nambari moja wa raisi yule yule ambaye alimpinga kwa nguvu zake zote huku raisi huyo akiwa hajabadilisha chochote katika staili yake ya uongozi zaidi ya kumpa cheo yeye Shamuhuna.

Kwa hivyo, hili halishitushi sana. Ikiwa kweli huu ni msimamo wa Shamuhuna tu, basi hiyo ni moja miongoni mwa njia nyingi zake nyingi za kujiwekea nafasi katika serikali ya Umoja wa Kitaifa ijayo (kama yaja). Si ajabu kwamba yeye akawa miongoni mwa wajumbe wa Kamati ya Maandalizi ya Uapishwaji wa Serikali Mpya ya Umoja wa Kitaifa, maana alivyo mzuri wa kumeza matapishi yake, akajiramba midomo, akajifuta kwa tissue kisha akakutizama machoni kana kwamba hajafanya kitu, ni ajabu kabisa!

Nimalizie makala hii kwa kurudia tena na tena umuhimu na, kwa kweli, ulazima wa wananchi wa Zanzibar kuletwa pamoja na kushirikiana katika uendeshaji wa nchi yao. Na kama ambavyo wengi wameshahitimisha, serikali ya pamoja ni kwa maslahi hayo. Maslahi ya Zanzibar na watu wake.

Ni makosa sana kudhani kwamba, ikiwa itaundwa serikali ya aina hiyo, basi ni CUF ndio watakaokuwa washindi. Hapana. Hali ilivyo sasa Zanzibar, sote tumeshindwa. Nchi yetu imesimama. Hata kwa kulinganisha tu baina ya pande hizi mbili za Tanzania, yaani Bara na Visiwani, basi Zanzibar imeoza.

Na hoja si kwamba, kuendelea mbele kwa Bara kunatokana na serikali ya umoja wa kitaifa, lakini ni kwa kuwa kuna namna ya maelewano ambayo Zanzibar hayapo. Na kwa kuwa chanzo cha kukosekana kwa maelewano hayo Zanzibar ni kuwatenga watu nje ya mduara wa utawala, basi dawa ni kuwashirikisha. Si kwa maslahi yao tu, bali kwa maslahi ya taifa.

Ni bahati mbaya sana kwamba ni CUF tu ndio wanaosikikana ‘kulipigia debe’ hili na hivyo kuonekana wao tu ndio watakaonufaika nalo, lakini, waungwana, hii Zanzibar ni yetu sote. Kuwa CUF hakumfanyi mtu kuwa pungufu ya Mzanzibari na wala kuwa CCM hakumfanyi kuwa zaidi yake. Tuzivunjeni kuta zilizotugawa kwa kujenga kuta za kutuunganisha!

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.