Mtazamo wa kihistoria unaotumiwa na wahafidhina wa Zanzibar kuhalalisha upinzani wao kwa hoja ya Maridhiano na Umoja wa Kitaifa una mapungufu makubwa. Ikiwa hoja ni kwamba Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF), kama vyama viwili vikubwa na pekee vinavyoongoza siasa za Zanzibar, haviwezi kuridhiana na kushirikiana kuongoza nchi hii kutokana na kuchimbukia katika asili zinazokinzana, basi upungufu wa kwanza ni kwamba, hoja hii haiangalii historia katika uhalisia wake.

Msukumo wa kihistoria (historical force) ambao ndio uliozaa mjengeko wa kijamii na kitamaduni (socio-cultural structure) wa Zanzibar unazungumza hadithi tafauti. Kwamba Wazanzibari ni watu mchanganyiko na kwamba kupitia mchanganyiko huo ndipo maisha yao yanapokwenda mbele katika kila nyanja – kisiasa, kiuchumi, kijamii na kitamaduni. Kila mara, mwenendo wa siasa za nchi hii zilipodharau au kukandamiza dhati hii ya mchanganyiko, basi mustakabali wa visiwa hivi ulitiwa rehani na kuingizwa katika majaribu makubwa. Kwa mfano, hakukuwa na haja ya kufanyika Mapinduzi ya 1964 ikiwa wafanya siasa wa wakati huo, kutoka pande zote, waliizingatia dhati hii.

Pili, hata kwa kutumuia hayo hayo mapokezi ya historia wanayoyaamini wahafidhina wetu, bado historia hiyo si sehemu salama kwao kujifichia, maana ni gofu lililojaa woga, kujishuku na kutokujiamini. Bahati mbaya kwao ni kuwa gofu hili lina mlango mmoja tu wa kutokea ambao umeandikwa: “Maridhiano na Umoja wa Kitaifa”. Mwangwi unaosikika ndani, kwa hakika unawafukuza wasikae gofuni humo. Ni mwangwi wa matendo yao. Kwa hivyo, ni ama kupita katika mlango huu au ni kubakia ndani ya jengo hilo wakawa wamekwama na kuikwamisha nchi katika khofu, woga na kutokujiamini kama hivi ilivyo sasa.

Nitafafanua. Kwanza, msimamo wa wahafidhina hao wa kuyasahaulisha yaliyopita (kama ulivyojadiliwa katika makala iliyotangulia) una makosa mengi ya kisayansi na hauwezi, hatimaye, kuifikisha Zanzibar popote zaidi ya hapa penye mfundo na mkwamo wa kisiasa na kiuchumi. Miongoni mwa makosa hayo ni kujengwa kwake juu ya imani kuwa kusahau kunamaanisha kufuta (delete) sehemu fulani ya taarifa zilizomo kwenye kumbukumbu ya mtu.

Usahihi ni kwamba, hata taarifa zinapokuwa zimesahauliwa, sio kwamba zimetupwa katika debe la takataka (dustbin), ambako haziwezi kupatikana tena, bali huwa zipo mahala fulani kwenye akili ambapo zinakingwa na aidha kizuizi-awali (intro-active inhibition) au kizuizi-tamati (retroactive inhibition). Vizuizi hivi navyo pia ni taarifa lakini huwa zimepewa kipaumbele zaidi kuliko ile taarifa nyengine.

Mwanafunzi aliyefahamu vyema somo la Mantiki, kwa mfano, anaweza kulisahau somo hili ikiwa amepokea taarifa nyengine ya kufiwa na mzazi wake, maana ile nafasi ya taarifa ya mwanzo (Mantiki) sasa inatawaliwa na taarifa mpya (kifo cha mzazi), ambayo imekuwa nzito zaidi kwake.

Hiyo, hata hivyo, haimaanishi kuwa ile Mantiki imeshapotea. Madhali iliwahi kupokewa katika akili yake kupitia milango ya fahamu, basi ipo mahala fulani ‘mafichoni’ na kile kinachohitajika ni ‘kuifichua’ tu – kwa kwenda kwenye search engine, kwa kutumia lugha ya kompyuta.

Pili, kadiri wahafidhina hawa wanavyotumia historia kuhalalisha ukaidi wao kwa Maridhiano na Umoja wa Kitaifa, ndivyo wanavyokwenda wenyewe kwenye hiyo search engine na ku-click programu ya kufichua kumbukumbu, ambako hakuwasaidii kujenga hoja yao.

Miongoni mwa njia za kufichua kumbukumbu kutoka kwenye akili ni kuyarejearejea maneno muhimu (key words) ya taarifa yenyewe (kama kauli ya Rais Amani Karume kwamba mapanga ya ’64 yangalipo inapoungana na mauaji ya Januari 2001), kupata taarifa zinazofanana (familiarization) nayo (kama kudai kwake kwamba ameombwa na wazee agombee tena uraisi kunakofanana na madai kama hayo ya mtangulizi wake, Salmin Amour, na fununu za kuirudisha Afro-Shirazi Party-ASP) na au kufuatana kwa taarifa (serialization) zenyewe (kama mlolongo ulioanza na Ali Juma Shamuhuna kupinga mazungumzo, kisha Samia Suluhu na kisha Karume mwenyewe ukihusishwa na mlolongo wa matukio kama hayo kuelekea kuchafuka kwa hali ya kisiasa Zanzibar mwaka 1984 na fununu za kuvunja Muungano). Kumbukumbu zote hizi haziwasaidii chochote wahafidhina hawa.

Tatu, kwa kuwa hiyo ndiyo historia ya Zanzibar na hayo ndiyo makovu yake, na kwa kuwa jitihada yoyote ya kuendelea kujifungia kwenye gofu hili la historia ni kujihalalishia vitisho, woga na kutokujiamini, basi yeyote mwenye akili timamu na dhamira njema kwa nchi hii, hataupa mgongo mlango wa Maridhiano na Umoja wa Kitaifa Zanzibar, maana ndio ‘utakaomtoa’ tu.

Mwenye akili timamu Zanzibar, hasa akiwa kwenye nafasi ya uongozi na kundi la wafuasi, atatafuta njia muafaka ya kuifanya historia imsaidie kupiga hatua mbele kama kiongozi wa watu anayejiamini zaidi. Na ni mwangwi ule wa kwenye gofu alimojifungia ndio unaomwambia hivyo. Ndio unaomfukuza: “Toka humu. Pita kwenye mlango wa Maridhiano na Umoja wa Kitaifa, uende zako!”

Nne, mtazamo wa kihistoria hauwezi kuzalisha wahafidhina, maana busara yake inasema kitu tafauti na ung’ang’anizi (rigidity) wa mambo. Inasema kuwa kujuwa tukuendako ni kwa kujuwa tutokako na kupaelewa tulipo. Na ili hilo lifanyike, ni lazima tukumbuke na tujifunze kwa kukumbuka huko. Kwamba ikiwa kuna mabaya yoyote yaliyotutokezea, basi tupate somo la kujifunza yasijirudie tena.

Historia ya Zanzibar ni shuhuda wa ubaguzi na matokeo yake mabaya, kukiwemo kudidimia kiuchumi, kielimu na kisiasa. Ukaidi hausaidii kitu, maana hata macho ya kawaida yanaona kwamba wenzetu wengi ulimwenguni, waliokuwa kama sisi, wameendelea kusonga mbele sana kwa sababu kile kinachotukuzwa Zanzibar (ubaguzi) kinadharauliwa huko. Anayeamini hasa juu ya mtazamo wa historia anakuwa mtu wa mwanzo kupingana na ubaguzi. Kwa hivyo, mtazamo wa kweli wa kihistoria huzalisha watu wenye uwezo wa kubadilika (flexibility) na sio ving’ang’anizi.

Labda tuseme kuwa wahafidhina wa Zanzibar wanaona, kwa mfano, kwamba mauaji ya 2001 yalikuwa ni tendo la kistaarabu na kwa hivyo la kutukuzwa na kurejewa tena na tena kila ikipatikana nafasi, lakini, kinyume cha hivyo, hawana sababu ya kukataa kwa Maridhiano. Au tuseme wanaona Muwafaka wa 2001 kilikuwa kitu kibaya sana kwao na hivyo ni jambo la kuepukwa kadiri inavyowezekana, lakini, kinyume cha hivyo, hawana sababu za kuukataa Umoja wa Kitaifa, hata kwa mtazamo huo huo wa kihistoria!

Tano, na mwisho, kwa mtazamo huu huu wa kihistoria, tuna uzoefu wa kilimwengu. Zanzibar si nchi pekee ulimwenguni iliyowahi kupitia historia kama hii. Ziko zilizopitia historia mbaya zaidi. Pia SMZ si serikali pekee iliyoingia madarakani kwa vurugu za umwagaji damu na kuishia kuyatumia madaraka hayo vibaya dhidi ya watu wake. Ziko zilizokuwa kandamizi kuliko hii.

Dunia imejaa mifano mingi. Utawala wa Adolf Hitler uliwatendea unyama mkubwa Mayahudi – karibuni nusu milioni walitiwa katika kambi za mateso, wengi wao wakafia humo na wengine wakakimbia nchi yao ya uzawa. Lakini watawala waliofuatia, kwa kujuwa machungu yanayobebwa na ndugu za wahanga hao na kuthamini maisha ya watu, wakaomba radhi na kufanya jitihada za kuwashirikisha tena Mayahudi katika mfumo wa maisha ya Ujerumani kisiasa, kiuchumi, kijamii na kitamaduni.

Katika nchi ya Afrika Kusini, siku za ubaguzi wa rangi zilisababisha machungu makubwa kwa jamii ya Waafrika weusi. Kitu cha mwanzo alichokifanya Nelson Mandela, baada ya kuingia madarakani, ilikuwa ni kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa na Tume ya Ukweli na Maridhiano. Leo hii machungu yanazidi kuyeyuka baina ya jamii hii moja yenye mchanganyiko kama wa Zanzibar.

Hiyo ndiyo mifano ya kuigwa Zanzibar. Kama Hitler alivyofanya, unazi wa kutisha umeshafanyika Zanzibar. Kama makaburu walivyofanya, ubaguzi wa hali ya juu ushafanyika Zanzibar. Na haya yanaendelea hadi sasa. Ni Maridhiano na Umoja wa Kitaifa tu ndiyo yatakayofungua nafsi zetu, kama alivyosema muombolezi mmoja katika mazishi ya karibuni ya P. W. Botha kuwaambia Waafrika Kusini: “Bury the history, before the history buries you”, yaani izikeni historia kabla historia haijawazikeni nyinyi.

Mifano ya kuigwa si ya akina Augustino Pinochet wa Chile, Sese Seko Mobutu wa Kongo Kinshasa au Slobodan Milosovic wa Yugoslavia. Yao ni mifano ya aibu, fedheha na majuto. Hatima ya tawala zao na wao binafsi si za kuzionea choyo. Hivi sasa Jenerali Pinochet anamalizia umri wake akilaaniwa na kila mstaarabu ulimwenguni. Salama yake ni kwamba, umri wake umemuombea asitiwe gerezani, lakini kiilivyo ni kwamba hukumu ya umma imeshamuangukia juu yake kutokana na unyama wake madarakani.

Naye Mobutu akawadhulumu raia wake kwa kila aina ya dhuluma – kuwaua, kuwatesa na kuwaibia. Mali yote ya Zaire aliikombakomba na kuihamishia nje. Rais wa nchi maskini kabisa akawa miongoni mwa matajiri wakubwa duniani. Lakini nini ulikuwa mwisho wake? Hata udongo wa nchi yake haukukisitiri kiwiliwili chake alipokufa, maana umma ulimfurusha na kwenda kufia ugenini. Kuna radda kama hiyo?

Katika uhai na utawala wake, Mobutu alikuwa amepewa na kuombwa kuzitumia fursa nyingi tu za kujisafisha, dogo zaidi likiwa ni hilo la kuwaleta pamoja Wakongomani, lakini badala yake alizidisha ufisadi na udikteta na, hivyo, kuisambaratisha nchi.

Ya Milosovic ni hayo hayo. Kwa kutumia jina la dola, aliwafanyia kila aina ya unyama raia wake waliokuwa na asili ya Serbia. Alipotakiwa azuie unyama huo, kwa kibri alisema kwamba hakuna mtu wa kumfundisha namna ya kuitawala Belgrade. Lakini naye alikufa dhalili akiwa mahabusu The Hague kwenye Mahkama ya Kimataifa.

Kwa hivyo, na wahafidhina wa Zanzibar nao wana mawili tu ya kujifunza kutoka mtazamo huu wa kihistoria: ama mkondo wa Ujerumani na Afrika Kusini katika utafutaji wa Maridhiano, Umoja wa Kitaifa na Hatima Njema au wa Milosovic, Mobutu na Pinochet katika kiburi, ujuwaji na mwisho mbaya. Kwamba Zanzibar ni kijisehemu tu cha ulimwengu huu mkubwa, ambao sasa umeshakumbwa na mabadiliko yanayolazimisha uwajibikaji, na wao hawawezi kujitenga kando. Ni ama waizike historia chafu wanayojidai kuitetea, au wangoje historia hiyo iwazike wao!

One thought on “Kwa nini Maridhiano na Umoja wa Kitaifa Zanzibar? 2”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.