Phobia ni ugonjwa wa kisaikolojia unaomfanya mwenye kuwa nao awe na woga na chuki za kupindukia zisizo na msingi dhidi ya kitu, mtu au hali fulani. Katika kamusi, neno hili limefasiliwa kama irrational fear and, or, irrational abhorrence. Na miongoni mwa fasili za neno irrational ni illogical, unreasonable, foolish, crazy, ridiculous, absurd, silly na unfounded. Siwezi kutafsiri kila moja ya fasili hizi, lakini itoshe kusema, kwa ufupi na kwa jumla, kuwa phobia ni aina moja ya uwendawazimu.

Na wendawazimu tuko wengi. Tumo miongoni mwetu, kwa mfano, tunaogopa buibui, kiumbe dhalili kama vilivyo, bila ya ushahidi ikiwa vidudu hivi vina madhara kwetu. Wengine tunaogopa kupanda ngazi ama kuangalia chini baada ya kupanda juu, kwa kisisi cha kuanguka. Tupo tunaoogopa kupita maeneo ya wazi, kama uwanja wa mpira, tukidhani ‘dubwana’ fulani linaweza kutokea hapo na kutubeba. Mara nyingi dhana hizi zina chimbuko lake katika sadiki-ukipenda, stereotypes.

Lakini phobia si kuogopa peke yake. Kwa kuwa ni woga usio na msingi, basi huja na chuki. Kwa hivyo, kwa kumuogopa jongoo kwa ujinga wetu wa kutomkumjua, kwa mfano, tunaishia kumchukia. Utamsikia mtu akisema: “dudu hili silipendi”, kumbe pia analiogopa. Hali hiyo hiyo hutokea kwa kwa kuwachukia watu wengine kutokana na giza hilo hilo la kutokuwajua.

Nakusudia kuwa nyingi ya chuki zetu kwa watu na, au, imani zao zinatokana na ujinga wetu. Tunaowajua kikwelikweli huwa aidha hatuwachukii kabisa na, au, hata tukiwachukia, hatuwaogopi. Vivyo hivyo kwa imani zao.

Lengo la makala hii si kuitambulisha phobia kwenu, bali kuitambulisha kwamba ipo na, kwa muktadha huu, ipo zaidi katika jamii za Magharibi (Ulaya na Marekani) kwa jina la islamophobia. Ugonjwa huu haujaanza leo katika dunia hiyo, lakini ni bahati mbaya sana kwamba licha ya kutambulika kwake, bado haujaponywa kwa kuwa ni ugonjwa unaopendwa na kukubalika na tawala za huko.

Miaka nenda miaka rudi sasa, woga unaoambatana na chuki dhidi ya Uislam na, au, kitu chochote kinachohusishwa nao, umekuwa ukienezwa kwa kila aina ya rangi na sura na tawala mbali mbali za Magharibi (bila ya shaka kwa maslahi ya kisiasa na kiuchumi ya familia za tawala hizo), huku nyuma ya islamophobia yenyewe kukiwa na ujinga wa kutokuujuwa kabisa huo Uislam wenyewe. Na sasa ugonjwa huu unaugharimu ulimwengu wote kwa jumla.

Mimi si muhubiri wa dini, na sikusudii kuigeuza makala hii kuwa kipande cha mjadala mpana wa kidini, lakini ni muumini na mfuasi wa itikadi inayotambua mdahalo na mdahala (dialogue and coexistence) baina ya watu wa dini tafauti na juu ya umoja wa imani zao kuliko tafauti zao. Nimelelewa na kukulia katika mazingira hayo hapa hapa Zanzibar.

Nazungumza dhidi ya islamophobia si kwa sababu ya Uislam wangu, la. Hata ningelikuwa muumini wa dini nyengine, bado itikadi yangu ya mdahalo na mdahala ingeliniambia kuwa islamophobia ni ugonjwa usio faida kwa dini yoyote ile, bali unaoitishia kuimomonyoa hata misingi ya hizo dini zenyewe.

Nazungumza dhidi ya islamophobia kwa kuwa ni saratani inayoila itikadi hiyo. Vita dhidi ya ugaidi vinavyoongozwa na Marekani vikiungwa mkono na nchi kadhaa za Ulaya, kwa mfano, licha ya kuwa pia na tafsiri kadhaa za kiuchumi na kisiasa, ni matokeo mamojawapo ya ugonjwa huu.

Vita hivi havijaisaidia dini yoyote na wala havitafanya hivyo milele. Vinaweza, yumkini, kutanua na kudhoofisha himaya za kisiasa na kiuchumi za tawala fulani, lakini kamwe haviwezi kutanua ama kudhoofisha himaya za kidini. Panapohusika imani za walimwengu kidini, vita hivi vinajenga kuta zaidi baina ya waumini wa imani tafauti kuliko kujenga madaraja baina yao.

Kauli ya karibuni ya Andres Tobias Rubio, afisa wa ngazi ya juu wa Jumuiya ya Ulaya (EU) anayeshughulikia masuala ya Afrika, Karibian na Pasifiki (rejea magazeti ya Mwananchi na The Citizen ya tarehe 01 Oktoba, 2006), kwamba Jumuiya yake iliendelea mbele kukubaliana na matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar wa mwaka 2005 hata baada ya kuwapo ushahidi unaonesha kinyume chake, kwa kuwa tu haikutaka kukiunga mkono Chama cha Wananchi (CUF) inachokihusisha na Uislam, ni mfano mmoja kati ya mingi ya kuwepo na kukubalika kwa ugonjwa huo wa islamophobia katika dunia ya Magharibi.

Kwa mujibu wa Rubio ni kwamba hata kama jumuiya yake iliyaona matatizo chungu nzima yalioukabili uchaguzi huo ambayo yaliuweka mbali na vigezo vya kuwa ‘huru na wa haki’, bado, kwa kuhofia kwake kwamba CUF ni chama kinachofuata siasa za Kiislam, ilifumbia macho matatizo hayo na ikayapa kisogo matakwa ya demokrasia, ili Zanzibar iendelee kuwa ya amani kwa watalii wa Ulaya kuweza kuitembelea.

Ni islamophobia. Baadhi ya wakati, hata wenye ugonjwa huu, hutumia sababu kengefu kukijengea ukuta wa ulinzi kile wakiaminicho. Katika hili, EU inaweza kuwa imetumia ile iitwayo deductive reasoning, yaani kusema kwa kuwa Wazanzibari wengi ni Waislam, na kwa kuwa Wazanzibari wengi wanaiunga mkono CUF, basi CUF ni chama cha Kiislam. Ikiwa hutumii kipawa chako vyema, unaweza nawe ukaambukizwa ugonjwa huo huo.

Lakini, ukiangalia hili katika uhalisia wake, utajuwa kuwa CUF inaungwa mkono zaidi Zanzibar kuliko sehemu nyengine za Tanzania, si kwa sababu za kidini, lakini kutokana na historia yake ya mapambano na namna ambavyo inauelezea Muungano wa Tanzania. CUF haitaki kuvunja Muungano lakini inazungumzia kuipa hadhi zaidi Zanzibar kuliko ilivyo sasa. Na hicho ni kitu kinachopendelewa na zaidi ya nusu ya Wazanzibari. Sasa kwa kuwa Zanzibar ina Waislam wengi, bila ya shaka CUF itakuwa na wanachama wake miongoni mwa Waislam hao. Si kwa kuwa wao ni Waislam, bali ni kwa kuwa wao ni Wazanzibari.

Vyenginevyo, ilikuwa iwatoe wapi na ifanyeje? Waanguke kutoka mbinguni? Au iwatake wabadilishe dini yao kwa kuwa tu sasa wanaingia katika mfumo wa siasa za vyama vingi, ambao waliozileta (Ulaya na Marekani) wanaiogopa na waniuchukia dini yao. Kwa kufanya hivyo, CUF nayo pia ingelikuwa na islamophobia!

Vyama vingi havikuja kuwapokonya watu dini zao. Wala Zanzibar haijapata kuwa na tatizo la imani kali za kidini katika historia yake. Licha ya kuwapo kwa mchanganyiko wa kitamaduni, hakujawahi kuwapo na ukereketwa wa kidini katika Visiwa hivi. Waumini wa dini zote wamekuwa wakiishi vyema huku kila mmoja akitambua na akiheshimu uwepo wa mwenzake. Zipo familia Zanzibar ambazo wanafamilia wake wanatoka dini tafauti na hilo halijapata kuwa tatizo kwao.

Lakini wenye islamophobia hawawezi kuliona na kulitambua hilo. Kwao wao, madhali CUF inaungwa mkono zaidi Zanzibar kwenye Waislam wengi, hitimisho ni kwamba CUF ni chama cha Kiislam na hivyo kuingia kwake madarakani kunamaanisha kuanzisha utawala wa Kiislam ambao, kwa mujibu wa akina Rubio wa EU, hupelekea machafuko na hali ya kukosekana kwa usalama katika taifa husika.

Jukumu la kuthibitisha kwamba CUF si chama cha kidini ni la wanachama na uongozi wa CUF wenyewe, lakini msimamo wa Jumuiya hii unatakiwa kuipa changamoto CUF kwa kuionesha sura halisi ya watu inaowatambua kama washiriki wazuri wa ujenzi wa demokrasia.

Kwamba hawa si wenza wazuri wala makini katika utetezi wa haki za walimwengu wenzao, maana vichwani mwao muna tatizo la islamophobia. Kwamba wanauogopa na kuuchukia sana Uislam kiasi ambacho akili zao zinagoma kufikiri na hivyo kwenda kinyume na hata misingi ya demokrasia wanayodai kuitetea kwa gharama zote.

Ikiwa baada ya damu yote kumwagwa, heshima yote ya Wazanzibari kuvunjwa na baada ya mateso yote waliyopata Wazanzibari huku wao wakishuhudia, bado walikwenda mbele kuhalalisha matokeo yanayotokana na uchaguzi huo, basi hawa si watu wa kuwaamini. Si watu wa kuwaamini, maana wako tayari kukuuza kwa bei rahisi ati kwa kuwa tu wewe ni Muislam.

Islamophobia ndio hasa unaosababisha kuzaliwa kwa ‘magaidi’ wanaojinasibisha na imani za dini ulimwenguni. Kwa nini wakajinasibisha na dini, ni kwa kuwa walipokandamizwa (au katika mfano huu, waliposalitiwa na kuachwa wateseke) dini yao ndiyo iliyokuwa kigezo. Waliangaliwa kwa mujibu wa dini zao na wakakandamizwa kwa mujibu wa dini hiyo, nao, katika kutafuta utetezi, hutumia dini hiyo hiyo. Hiyo, japokuwa si halali, ndiyo mantiki nyepesi kabisa ya ufurukutwa wa kidini.

Zanzibar ya sasa haiko tulivu (ikiwa hali ya sasa inaweza kuitwa hivyo) kwa kuwa CUF ilishindwa kuingia madarakani, bali ni kwa kuwa bado CUF imebakia kuwa kama CUF – chama cha siasa kinachotumia siasa kufanya siasa. Hilo limeipa CUF uhalali na, hivyo, mamlaka, miongoni mwa Wazanzibari walio wengi.

Siku CUF, kwa maana ya uongozi wake, itakapopoteza udhibiti wa siasa za nchi, huo usalama na utulivu anaozungumia Rubio pia utapotea. Kuwadhibiti na kuwaongoza watu waliovunjwa moyo na usaliti wa mara kwa mara (kama huu wa EU), ni kazi kubwa sana. Ni kazi ngumu inayofanywa sasa na uongozi wa CUF na inaonekana hadi sasa hakuna mbadala wake. Lakini usaliti ukiendelea, mbadala utakuwa hauepukiki.

Mara tu baada ya matokeo ya uchaguzi huo wa 2005, nikiwa nimeshuhudia kwa macho yangu yote yaliyotokea, niliandika shairi kulalamikia usaliti wa ulimwengu kwa wananchi wa Zanzibar ambalo nililiita ‘Mumetusaliti’. Sasa imesadifu kwamba kauli ya Rubio wa EU inashabihiana na baadhi ya beti za shairi hilo huru:

Twalia kwa mabalozi
Na muitwao waangalizi
Muloona kila kitu
Mukajifanya hamukuona
Mulosikia kila kitu
Mukajifanya hamukusikia
Mulojuwa kila kitu
Mukajifanya hamukujuwa
Mukafumba macho yenu
Mukageuza shingo zenu
Mkaziba masikio yenu
Na hata akili zenu
Zikagoma kufikiri
Kusudi mupate hoja –
Na haja ya kusaliti!

Basi tumejuwa
Kumbe vile haja yenu:
Tusagwesagwe, tupondwe
Tumalizwe, tuangamizwe
Na majeshi ya kigeni
Katika ardhi yetu
Muitwae nchi yetu
Muchimbe mafuta yetu
Rasilimali yetu na wenetu
Ndipo mukatusaliti!

Lakini nanyi mujuwe
Japo mulitusaliti
Kupigwa tukapigwa
Kufungwa tukafungwa
Tukakashifiwa, tukaibiwa
Sisi tuliweza kusimama
Kwa wingi na kwa umoja
Tukalinda kauli yetu
Ya kusema hapana
Hapana kwa ukoloni
Hapana kwa ujinga
Hapana kwa unafiki
Na hapana kwa usaliti!

Na sasa hivi tulivyo
Twachiria damu, jasho na usaha
Na nguo zetu mararu
Tuna njaa, kiu na ufukara
Tu wanyonge
Lakini
Bado tu hai
Hatuna khofu wala woga
Tuna nia na dhamira
Kuendelea kusema:
HATUTAKI
Nanyi
Endeleeni kutusaliti!

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.